Waliikuta mifupa yake kando ya kibanda chake cha muda katika kisiwa kisichokuwa na watu katikati ya Atlantiki. Baharia yule asiyejulikana jina lake alitunza kitabu cha mambo ya kila siku kilichoeleza kwa kinagaubaga mateso mabaya aliyopata kwa miezi minne. Alikuwa ametelekezwa pwani ya kisiwa cha Ascension na kundi la manowari za Kiholanzi chini ya kamanda mmoja katika mwaka wa 1725 kwa uhalifu wake fulani uliokuwa haujatajwa. Baada ya muda mfupi kupita, akawa akinywa damu ya kasa ili kuituliza kiu yake kali sana. Mateso ya mtu yule kimwili yalikuwa makali sana, lakini maumivu makubwa zaidi yanaonekana wazi katika kitabu chake cha mambo ya kila siku: yaani, ile hatia yake iliyomlemea kabisa.
Aliandika maneno yaliyomtesa sana kama haya: "Ni maumivu yaliyoje yanayowapata wanadamu wanaoziacha njia za haki, wakifurahia kuongeza idadi ya watu waliolaaniwa." Kutengwa kabisa kwa baharia yule katika kisiwa kile cha upweke kulitokana na hisia yake ya kutengwa mbali na Mungu. Hilo ndilo jambo ambalo mwishowe lilionekana kwake kuwa halivumiliki.
Wanadamu wamekuwa wakipambana na kutengwa huko mioyoni mwao tangu Adamu na Hawa walipo"jificha BWANA Mungu asiwaone kati ya miti ya bustani" baada ya kula lile tunda lililokatazwa (Mwanzo 3:8). Hisia mpya, ngeni, za kuona aibu, hatia, na hofu zikawalazimisha wale watu wawili, mume na mke, kumkimbia Mungu alipokuja na kuwaita. Hisia zile, kwa bahati mbaya, sasa zinafahamika sana kwetu.
Je, ni kitu gani kinachosababisha utengo huo kati yetu na Mungu?
“"Lakini maovu yenu yamewafarakisha ninyi na Mungu wenu; dhambi zenu zimeuficha uso wake msiuone"”
Ufa huo mkubwa unaowatenga wenye dhambi mbali na Mungu hautokani na Mungu. Mungu hakutimua mbio kumwacha Adamu na Hawa - wao ndio waliomkimbia yeye.
